Maonesho ya Nanenane kanda ya mashariki mikoa ya (Pwani, Dar es salaam, Tanga na Morogoro) yaliyoanza tarehe 01/08/2022, yamezinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Mstaafu awamu ya nne Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda leo tarehe 04/08/2022 katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere Mkoani Morogoro.

                                         

Maonesho haya ya kilimo, Mifugo na Uvuvi yamebeba kauli mbiu isemayo “Agenda 10/30 kilimo ni biashara shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, Mifugo na uvuvi”. Maonesho haya yamehudhuriwa na watu mbalimbali kama vile Viongozi wa serikali, mashirirka binafsi, taasisi mbalimbali, wadau wa Kilimo , Mifugo na Uvuvi, pamoja na wadau wa viwanda vya nyenzo za kilimo.

                                             

Akiongea wakati wa Hafla ya ufunguzi Mkuu  wa Mkoa wa morogoro Mhe. Fatma Mwasa amesema lengo kuu la maonesho haya ni kutoa elimu kwa Wakulima,wafugaji na wavuvi, Kujifunza mbinu mpya za kiteknolojia, Kuondoa migogoro kati  ya wakulima na wafugaji ili kufuga kwa tija pamoja na  Kukuza ujuzi na  uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Pia mgeni rasmi wa maonesho haya Waziri mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amesema anaipongeza kanda ya mashariki kwa kuandaa maonesho kwa kiwango kinachoridhisha na kupata nafasi ya kutembelea mabanda katika mbalimbali na kujifunza teknolojia nzuri za kilimo,mifugo na uvuvi.

                                               

Pamoja na hayo, mgeni rasmi  alipata fursa ya kutembelea banda la chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA),  akiongozwa na makamu mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda na kuona mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo pamoja na udhibiti wa viumbe hai waharibifu  kama vile panya mashambani.