Watafiti kutoka Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu, SUA, wanaendelea na tafiti mbalimbali Mkoani Iringa, Wilaya ya Iringa Vijijini, Kata ya Isimani, Kijiji cha Kising’ha. Utafiti unafanyika katika Kituo cha Majaribio ya Kilimo cha Uyole ikiwa ni mwendelezo wa tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi hii. Udhibiti ulioanzishwa unalenga kupunguza panya waharibifu kwenye mashamba ya mahindi, alizeti na maharage kwa kutumia ndege aina ya bundi.
Lengo kuu ni kutumia njia za kibaiologia na ikologia ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina na kuonyesha mafanikio ili kupunguza tatizo la panya mashambani na nyumbani.
Prof Loth Mulungu ambaye ni Mtafiti toka Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu,SUA, ameeleza kuwa kwa kutumia ndege aina ya Bundi kupambana na panya waharibifu wakulima wataondokana na tatizo la mbegu zao kuharibiwa na panya mashambani. Ameeleza pia ipo haja ya kuendelea kuelimisha jamii kuhusu faida za bundi ambao chakula chao kikuu ni panya. Kuwepo kwa bundi kutawezesha kupunguza idadi ya panya mashambani, hivyo jamii itafaidika kwa kuondokana na matatizo ya panya wharibifu. Tafiti zinaonesha kuwa Bundi mmoja ana uwezo wa kula zaidi ya panya kumi (10) kwa siku. Ndani ya msimu mmoja bundi wanaweza kula mamia ya panya na kupunguza athari za uharibifu wa mazao unaosababishwa na panya mashambani.
Bundi ni ndege ambae huruka usiku ili kuwinda wanyama wadogo wadogo kama panya, wadudu na hata ndege wengineo. Uwezo wa bundi kuona usiku ni mkubwa na anaweza kuruka umbali mkubwa akiwa mawindoni. Mbali na mtazamo hasi wa jamii duniani kuhusu bundi, utafiti unaonyesha kuwa bundi ni ndege asie na madhara yoyote kwa binadamu bali ana faida kubwa kwa mkulima. Mbali na kupunguza panya waharibifu shambani, huondoa pia uwezekano wa milipuko ya magonjwa yanayosababishwa au kubebwa na panya kwa vile idadi ya panya itapungua.