Watafiti Kutoka Kituo Cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu (SUA) wamefanya ziara ya kitafiti wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma tarehe 9/4/2021 ambapo wameweza kuwatembelea wanafunzi wa shahada ya Uzamivu na shahada ya Umahiri kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo wanaofanya tafiti zao mkoani humo.
Ziara hii imelenga kusimamia ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za kitafiti zinazofanywa na wanafunzi wa SUA, pia kuangalia tabia, ikolojia na aina za magonjwa yanayoweza kusababishwa na Panya wanaopatikana katika ukanda huo wa kaskazini mwa ziwa Tanganyika.
Watafiti hao wakiongozwa na Prof. Apia Massawe pamoja na Prof. Loth Mulungu wameweza kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la hifadhi ya msitu wa Kakonko ambapo tafiti hizo zinafanyika na kuweza kushauri baadhi ya mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa takwimu (data)mbalimbali zinazotakiwa ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa kwenye tafiti lengwa.
Tafiti zinazofanywa katika mkoa huu zinalenga kuangalia magonjwa yanayoweza kutoka kwa Panya kwenda kwa binadamu na wanyama wengine pia kupata njia ya kuzuia magonjwa hayo yasilete madhara katika jamii husika.